Mkuu wa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, ameanza kutekeleza mapendekezo na msimamo wa Serikali kusimamia migogoro ya ardhi iliyokithiri kata ya Mapinga ambapo imeweka rekodi ya kata inayoongoza kwa migogoro hiyo nchini.
Ameeleza katika hatua hiyo inayochukuliwa na Serikali, wanatarajia kutenda haki ,ila hatoweza kumvumilia yeyote atakayeleta chokochoko na kujiona yupo juu ya Serikali .
Akizungumza katika mkutano wa wananchi wa kata ya Mapinga, Bagamoyo Mkoani Pwani, Kunenge alielezea nia ni kumaliza migogoro,kuipanga kata hiyo kwa kufuata sheria kwani haiwezekani Mapinga isishikike.
Amesema ,kuanzia Februari 2, mwaka huu, atafika Mapinga ,akiwa na orodha ya watu 20 wenye migogoro,na wataenda mguu kwa mguu kwenye maeneo husika na kufanya Maamuzi ili kila mmoja aridhike, ambapo ameongeza zoezi hilo litaendelea wahusika wakiendelea kutaarifiwa hadi watakapomaliza migogoro yote iliyofikishwa kwa Waziri.
“Mtakumbuka nilifika hapa na William Lukuvi (mb) aliyekuwa Waziri wa Ardhi kutatua kero za ardhi mkoa wa Pwani na alisema wazi takwimu inaonyesha hii ndio kata inayoongoza kwa migogoro ya ardhi nchini”
“Aliunda kamati ya watalaam, akiwemo Kamishna wa ardhi mkoa,na mara ya pili nilikuja tena nikiwa na Angelina Mabula Waziri wa Ardhi,ambapo alieleza Serikali imepokea mapendekezo ya kamati na ndio msimamo wa Serikali”amefafanua Kunenge.
Amesema ameanza utekelezaji,Mapinga ni kata tofauti na maeneo mengine ,kwingine ni rahisi kuzitatua migogoro ya ardhi Lakini kwa kata hiyo migogoro ni migumu ,ya muda mrefu na migogoro mingine tayari ipo mahakamani.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa alieleza Kuwa ,katika utekelezaji huo hatoingilia mahakama kwa maana ya Maamuzi yaliyofanywa na mahakama.
“Ila endapo kutakuwa na masuala ya maadili kwa waliopewa dhamana ya kufanya Maamuzi yaani watendaji,mnitaarifu nitashughulikia kwakuwa Mimi ni Mwenyekiti wa kamati ya maadili ya mahakimu Nina uwezo nao ,nitashughulikia ili haki itendeke” amesema.
Kunenge ameeleza, atahakikisha wananchi wanakuwa salama na amani ,Sasa atakaeona yeye ana mapembe na yupo juu ya sheria asije kumlaumu."
Awali mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash ,amesema kuna changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi .
Ameelezea kata hiyo inaongoza kwa uuzaji holela na uvamizi uliokithiri ambapo taarifa za migogoro hiyo zilishafika mkoa ,ikaundwa timu ndogo kuangalia utaratibu utakaotumika ili kusuluhisha na kutatua changamoto hiyo.